Malaki 3: 13-18
13Maneno yenu yamekuwa magumu juu yangu, asema BWANA. Lakini ninyi mwasema, Tumesema maneno magumu juu yako kwa namna gani? 14Mmesema; Kumtumikia Mungu hakuna faida; na, Tumepata faida gani kwa kuyashika maagizo yake, na kwa kwenda kwa huzuni mbele za BWANA wa majeshi? 15Na sasa twasema ya kwamba wenye kiburi ndio walio heri; naam, watendao maovu ndio wajengwao; naam, wamjaribuo Mungu ndio waponywao. 16Ndipo walio mcha BWANA waliposemezana wao kwa wao. Naye BWANA akasikiliza, akasikia; na kitabu cha ukumbusho kikaandikwa mbele zake, kwa ajili ya hao aliomcha BWANA, na kulitafakari jina lake. 17Nao watakuwa wangu, asema BWANA wa majeshi, katika siku ile niifanyayo; watakuwa hazina yangu hasa; naami nitawaachilia, kama vile mtu amwachiliavyo mwanawe mwenyewe amtumikiaye. 18Ndipo mtakaporudi, nanyi mtapambanua kati ya wenye haki na waovu, kati ya yeye amtumikiaye Mungu na yeye asiyemtumikia”
Kuna watu, na pengine nawe ni mmoja wao, ambaye baada ya kukaa katika maisha ya kumtafuta Mungu na kuona hapati alichotarajia, hugeuka na kuanza kulalamika. Hulalamika kwa kuona kama amejitaabisha bure katika kujiepusha na uovu wa dunia hii. Huona kama amejizuwia kutenda maovu pasipo kuwa na faida. Anaweza hata kushawishika anapowaona watu wakifurahia dhambi akajiona yeye anaishi maisha ya huzuni pasipo na sababu [ingawa kumcha Bwana ni furaha kubwa].
Pengine mtu amekuwa akifunga na kuomba ili jambo fulani litokee. Na kinyume chake akawaona wale ambao hata jina la Yesu halijawahi kutamkwa vinywani mwao ndio wanaofanikiwa. Ndio wanaojenga majumba makubwa, na wengine kuyaita kwa majina yao; akaona wale wanaotoa rushwa maofisini ndio wanaoongezewa mishahara na kupandishwa vyeo, huku yeye akiwa ameishikilia haki, yuko katika nafasi ile ile.
Yawezekana kuna mtu amekuwa anasumbuliwa na ugonjwa fulani kwa muda mrefu, ameomba sana lakini ugonjwa huondoki. Halafu akiangalia upande wa pili anaona kuna mtu ambaye alikwenda mara moja tu kwenye maombezi kisha akapona; na baada ya kupona mtu huyo alirudi tena dhambini, yaani kupona kwake ndio kumempa nguvu zaidi ya kutenda maovu. [3:15]Huyo aliyekuwa anamjaribu Mungu ndiye amepona halafu yeye bado anaumwa!
Sikiliza Neno la Mungu lisemavyo katika ule mstari wa 16 “Ndipo walio mcha BWANA waliposemezana wao kwa wao. Naye BWANA akasikiliza, akasikia; na kitabu cha ukumbusho kikaandikwa mbele zake, kwa ajili ya hao aliomcha BWANA, na kulitafakari jina lake”
Jambo muhimu kulifahamu hapa ni kitu walichosemezana wao kwa wao, hao wamchao BWANA. Lakini bila shaka hao wamchao Bwana walisemezana juu ya ukuu wa Mungu! Walifarijiana na kutiana moyo kuwa japo wanapita katika mapito bado BWANA Mungu ndiye nguvu yao. Walifarijiana kwamba hata kama walichofunga na kukifanyia maombi hakikutokea bado BWANA Mungu ni tumaini lao!
Ni kama tu walivyosemezana akina Shadraki, Meshaki na Abednego kuwa hata kama BWANA Mungu asipowaokoa katika lile tanuru la Moto lakini wao hawakuwa tayari kuisujudia ile sanamu ambayo mfalme Nebukadreza aliyokuwa ameisimamisha! [Daniel 3].
Wamchao waliposemezana BWANA alisikiliza na akasikia wakiongea maneno yenye kuelekeza kwake tumaini lao lote. Baada ya BWANA kusikia maneno hayo pale pale kitabu cha ukumbusho kiliandikwa mbele zake wa ajili yao kwa kuwa walisemezana maneno mema huku waliendelea kulitafakari jina lake!
Tusidanganyike! Kumtumikia BWANA Mungu kuna faida. Kuokoka kuna faida. Waache wanaofanikiwa kwa njia za ufisadi wafanikiwe. Waache wanaochekelea katika furaha ya dhambi, ambayo ni ya kitambo kidogo sana, waendelee[Ebrania 11:25]. Waache wanaojiunga katika imani potofu kwa ahadi za utajiri waendelee, maana siku itakapofika utajiri huo hautakuwa na msaada wowote kwao. Waache wanaotafuta uponyaji kwa njia zisizo za ki-Mungu waendelee maana iko siku ambayo itakuwa kama vile magonjwa hayo yamerudi yote kwa wakati mmoja!
Lakini pia iko siku BWANA ataondoa tabu yako. Pengine ameacha shida, ugonjwa au adui huyo aendelee kukusumbua kwa kusudi akufundishe jambo. Pengine ameacha ili akujaribu moyo wako umeweka wapi msingi. Pengine ameacha ili akujaribu unataka mema tu toka kwake au hata mabaya? [Ayubu 1:10]. Yawezekana ameacha ili akuone kama uko tayari kufa kwa ugonjwa huku bado sifa zake zikitoka kinywani mwako na wala hautamkufuru. Pengine amaecha hayo ili uendelee kunyenyekea. [2Kor 12:7]. Pengine ameacha hayo ili akutukuze, akufanye mfano wa Ayubu, ili uwe mfano wa kuigwa katika vizazi na vizazi!
Hebu tuendelee kumtumaini BWANA Mungu. Tuendelee kumuisha yeye. Tuendele kujitia nguvu katika yeye. Tunapokutana tusemezane maneno ya Neema hii aliyotupatia, Neema ya Wokovu. Tunapokuata tuliitie jina lake. Hapo ndipo tutaweka rekodi mbinguni! Loh! Ni fahari iliyoje mcha Mungu kuongea huku duniani kisha mambo hayo yakaandikwa mbinguni!
Kumcha BWANA kuna faida! Tudumu katika hilo kwa kuwa katika siku ile tutakuja kutambulika kama tulikuwa tunamcha BWANA Mungu, kama kweli tutadumu katika kumcha Yeye! Na hapo ndipo kutakuwa na malipo kwa wenye haki, Uzima wa milele na waovu, adhabu ya milele!
Mungu atusaidie!
Filed under: NENO
