Sisi tunaomwamini Bwana Yesu kama Bwana na Mwokozi wetu, Neno la Mungu linatuambia ya kwamba Yeye yuko ndani yetu na sisi tumo ndani yake, pia linatuambia tumeketishwa pamoja naye katika ulimwengu wa roho juu sana kupita falme na mamlaka zote (Waefeso 1:20-23, 2:6). Neno la Mungu pia linasema aliyeko ndani yetu ni mkuu kuliko aliyeko katika dunia, yaani ibilisi (1 Yohana 4:4).
Kama vile hiyo haitoshi Bwana Yesu alituambia hivi:
Tazama nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na ng’e na nguvu zote za yule adui na wala hakuna kitakachowadhuru – Luka 10:19 SUV
Hivyo hatuna sababu yoyote ya kumwogopa ibilisi shetani, mapepo na makuadi wao, maana tayari wameshawekwa chini ya miguu yetu. Tunao ushindi, naam zaidi ya ushindi kwake yeye aliyetupenda hata akajitoa kwa ajili yetu, yaani Bwana Yesu mwokozi wetu! Kama watenda kazi pamoja na Kristo, tusisite kuyatumia mamlaka tuliyonayo ndani yake kuwafungua wote wanaoteswa na iblisi kila hitaji linapojitokeza.
Mpendwa, tembea katika mamlaka uliyopewa na Bwana Yesu, wewe ni mwakilishi wake hapa duniani, wewe ni balozi wake popote pale ulipo, na kama balozi, mamlaka ya mbinguni yako pamoja nawe. Hivyo basi tuyatumie mamlaka tuliyopewa kuuharibu ufalme wa iblisi na kazi zake ili kuueneza na kuujenga ufalme wa Mungu!
Mbarikiwe na Bwana Yesu!
–Patrick
Filed under: NENO
