Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu – Warumi 12: 2
Na mfanywe wapya katika roho ya nia zenu; – Waefeso 4: 23
Neno la Mungu linatukumbusha sisi tunaomwamini Bwana Yesu kama Bwana na Mwokozi wetu ya kwamba, ili tuweze kuishi maisha ya ushindi ni lazima tuendelee kufanywa upya katika roho za nia zetu kila siku, au kwa maneno mengine, mawazo na mitizamo yetu inabidi ibadilike kuendana na Neno la Mungu linavyosema. Tusikubali kuishi tena kama watu wasio na tumaini, Neno linatuambia ya kwamba Mungu anatutakia mema siku zote za maisha yetu ( Yeremia 29: 11, 3 Yohana 1: 2).
Labda nitoe mfano mmoja halisi; tuseme umekabiliwa na tatizo la ugonjwa, badala ya kuwaza na kusema kama wengine wasiomjua Mungu maneno kama vile “ugonjwa huu utaniua”, au “huu ni ugonjwa wangu”, au “kila mwaka lazima niugue hivi”, badili kauli yako ukatae huo ugonjwa na dalili zake zote ukikiri Neno linavyosema “kwa kupigwa kwake mimi nimepona”, “Jehovah Rapha, Bwana ndiye mponyaji wangu”. Kumbuka pia Bwana Yesu alitupa mamlaka akisema “waniaminio…wataweka mikono juu ya wagonjwa nao watapata afya”.
Tunazo ahadi nyingi tu katika Neno la Mungu kuhusu uponyaji, mahitaji na mambo mbalimbali, yaamini na kuyakiri uushuhudie mkono wa Mungu maishani mwako! Kwa kifupi, kufanywa upya katika roho ya nia zetu, ni kitendo cha kudhamiria KULIAMINI Neno la Mungu KULIKO mazingira yetu. Tutambue ya kuwa Mungu si mwanadamu hata aseme uongo, hivyo basi Neno lake siku zote ni kweli (Warumi 3:4) na sisi tuna haki na kila ahadi kwa sababu ya kazi kamilifu ya ukombozi aliyoifanya Bwana Yesu pale msalabani.
Tuelewe ya kwamba sisi hatuko peke yetu tena, tunaye Roho Mtakatifu ndani yetu naye atatuwezesha kuliamini Neno linavyosema na kukubaliana nalo kuanzia kwenye mitazamo yetu, mioyo yetu na hatimaye kwenye kauli zetu na matendo yetu, ili tuishi maisha ya ushindi kwa ajili ya utukufu wa Mungu. Amen!
Mbarikiwe watakatifu wa Bwana Yesu,
–Patrick
Filed under: NENO
